|
WANAUME WATELEKEZA WATOTO WENYE ULEMAVU ARUMERUBaadhi ya walemavu waliopokea misaada ya baiskeli na wageni waliohudhuria hafla hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na Mbunge Catherine Magige na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Maongela.
Baadhi ya misaada ni baiskeli kwa walemavu na mitaji ya biashara kwa
vikundi vya wanawake wa Wilaya za Longido na Arumeru, kutoa misaada ya
ofisi za UVCCM na UWT, Longido, Arumeru na Mkoa wa Arusha na kuwalipia
faini wafungwa waliokuwa jela baada ya kushindwa kulipa faini
walizohukumiwa.
|
*Wanawake wasukumiwa mzigo
Tatizo
la wanaume kuwatelekeza watoto wao wenye ulemavu, limetajwa kukithiri
katika Kijiji cha Ambureni, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na JAMHURI hivi
karibuni, umebaini kuwapo kwa familia zaidi ya 15 zenye watoto walemavu
zilizotelekezwa na waume, hivyo wanawake kuachiwa mzigo wa kuzilea.
Tabia
hiyo imesababisha familia hizo kuishi katika mazingira magumu ikiwa ni
pamoja na kuishi katika nyumba za kupanga, huku zikiwa hazina kazi za
kujipatia kipato. Mateso yanayowakabili wanawake hao yanatokana na
kujifungua watoto wenye ulemavu, kwani bila kujifungua watoto hao
wangeendelea kuishi na waume zao.
Zeana
Athuman, mkazi wa Ambureni ambaye pia ni mwanawake aliyeathirika na
hali hiyo, anasema mume wake aliondoka nyumbani baada ya kujifungua
mtoto mwenye ulemavu.
“Baada ya kujifungua mume wangu alitoroka nyumbani na akaniacha nikiwa peke yangu katika hali ngumu kimaisha,” anasema Zeana.
Alijifungua mtoto mwenye ulemavu wa kutoona, kutotembea, kutosikia na kutozungumza.
“Mume wangu alimwona mwanangu kama mkosi ndani ya familia, alinikimbia mtoto akiwa na mwezi mmoja,” anasema.
Anaongeza
kwamba tangu mumewe amkimbie ni miaka 11 imepita sasa, jambo
linaloendelea kufanya maisha yake na mtoto wake kuwa magumu zaidi.
Zeana
anasema ili kukidhi mahitaji yake na mtoto wake kwa siku, analazimika
kumuacha mwanaye huyo kwa majirani aweze kutafuta fedha za kujikimu.
Changamoto iliyopo ni kwamba muda mwingi mtoto huyo hufungiwa ndani
wakati wote ambao mama yake hutoka kwenda kutafuta riziki.
JAMHURI
pia inakutana na mtoto anayetajwa kwa jina moja la Terezia (6) mwenye
ulemavu anayeishi na bibi yake. Taarifa zinasema baba mzazi wa mtoto
huyu aliondoka nyumbani hapo baada ya kuona mtoto wake ni mlemavu.
Wakati
baba akiwa amemtoroka mwanaye, mtoto huyu anatajwa kuwa katika
mazingira magumu zaidi kwani hata mama yake naye hulazimika kuondoka
nyumbani na kumuacha akiwa peke yake.
“Mtoto
huyu alizaliwa akiwa mzima, baada ya miezi saba hali yake ilianza
kubadilika akawa haoni wala kusikia ndipo baba mzazi alipoamua kuondoka
nyumbani.
“Mama mzazi naye alianza kumficha ndani kwa madai kuwa anaogopa watu kumsema amezaa mtoto mlemavu.
“Baada
ya majirani kugundua tatizo hilo waliamua kwenda kumtoa ndani kwa nguvu
na kuanza kumshindisha nje kama watu wengine,” anasema bibi wa Terezia
bila kutaja jina lake.
Kutokana
na changamoto zinazowakabili wanawake wenye watoto walemavu kijijini
hapo, hatimaye wamebuni mbinu za kulea watoto wa watu (yaya) ili wapate
kipato cha kuendesha maisha yao.
Mwalimu
wa kituo cha kulelea watoto wenye ulamavu katika Shule ya Msingi
Moivaro wilayani Arumeru, Leah Ndaga, anataja changamoto zinazowakabili
katika kazi hiyo. Mwalimu Leah anasema kwamba kwa muda mrefu sasa
wananchi wamekuwa wakibeza aina ya kazi wanayoifanya kwa madai kuwa
wanapoteza muda kukaa na watoto wenye ulemavu.
“Tunatoa
elimu kwa jamii na maeneo yanayotuzunguka kuwa watoto hawa ni sehemu ya
jamii yetu. Tunaiomba jamii iwachukulie kama sehemu yao isiwatenge
badala yake iwasaidie wanapohitaji msaada ukiwamo wa kwenda shuleni,”
anasema.
Wakati
wakiendelea na juhudi za kusaidia miundombinu ya kwenda eneo moja hadi
jingine, kituo hicho kina watoto 47. Kati ya hao, watoto watatu wana
ulemavu wa macho huku wengine wakiwa na ulemavu wa kutosikia, kutoongea
na kutotembea.
Mwenyekiti
wa Kitongoji cha Msovero, Sioni Mathayo, akizungumzia changamoto hiyo
anasema imekuwa vigumu kuwasaidia watoto hao kutokana na kutokuwa na
kipato cha kutosheleza mahitaji.
“Serikali
ya kitongoji hatuna mafungu ya kusaidia watoto walemavu. Tunaomba
viongozi wajaribu kuangalia upya jinsi ya kuziwezesha serikali za
vitongoji ambazo zipo na wananchi,’’ anasema Mathayo.
Pamoja
na kutokuwa na bajeti, Mwenyekiti huyo anabainisha kuwa kama kiongozi
alichukua jukumu la kupeleka matatizo hayo kwenye uongozi wa juu ili
kupata msaada wa namna ya kuwabana wanaume hao wasizikimbie familia zao.
Anasema
juhudi nyingine zinazofanywa ni za kuwapatia msaada kupitia Kituo cha
Aston Vision kilichopo kijijini hapo, ambacho hutoa elimu kwa watoto
yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Mwasisi
wa kituo hicho, Aston Simoni, anasema lengo la kuanzisha kituo hicho
lilitokana na kijiji hicho kuwa na watoto wengi wenye ulemavu na
wanaoishi katika mazingira hatarishi.
“Hapa
tunapata msaada kutoka kwa wadau wa nje na ndani ya nchi ambao
hutusaidia chakula, magodoro na dawa za kuongeza vitamini kwa watoto
yatima na wale wenye walemavu.
Kwa hisani ya gazeti la Jamhuri
|