FLASH

Wednesday, October 24, 2012

HAYA NDIYO YALIYOMKUTA YAHAYA MOHAMED WA STAR TV

Yahya Mohamed wa Star TV asimulia alivyonusurika na ajali ya basi na jinsi alivyoona uchawi unavyohusika!

Mtangazaji mashuhuri wa Star TV Yahya Mohamed jana kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook amesimulia kisa cha kusimumua namna alivyonusurika na ajali mbaya ya basi alipokuwa akitokea Mwanza kwenda Dodoma. Hivi ndivyo alivyoandika:
“Mkasa huu unasisimua kidogo lakini pia unatia shauku ya kujifunza mengi kuhusu kafara nyingi za ajali za barabarani, Hebu fuatana nami katika mkasa huu mdogo ulionisibu na abiria wenzangu tukitokea Mwanza kwenda DODOMA.
Eneo hili ni kijiji cha Igogo kati ya Igunga na Nzega, eneo linalokaliwa na idadi kubwa ya wakulima na wafugaji wa makibila ya wasukuma.
Muda mfupi baada ya gari letu KIDIA ONE EXPRESS kukamilisha kuzibwa rejeta iliyotupa adhabu ya kukaa kwa zaidi ya masaa 3 eneo mbele kidogo ya mji wa Nzega, tulifanikiwa kutanzua kadhia hiyo na kuendelea na safari kwa kiasi cha mwendo wa kama dk 30 kabla ya kusikia kishindo kikubwa mithili ya Radi nzito ambayo radi ya aina hiyo ipiga huwa saketi zote za hadhari za mfumo wa umeme katika gridi ya taifa huzima kwa kuepusha maafa zaidi.
Kishindo hiki kiliniamsha katika usingizi mzito uliokuwa ukiambatana na ndoto ambayo ilionyesha nipo katika eneo kunanyesha mvua kubwa sana nikiwa na mtoto wangu Yasser na ghafla katika mvua hiyo kulipiga radi nzito ya ajabu ambayo ilinistua sana na kuhamaki.
Kama umewahi kuota ndoto ukastuka tukio likafanana na sehemu ya mwisho ya ndoto, ndilo jambo lililotokea hapa. Haikuwa Radi bali kishindo kizito cha kupasuka kwa tairi ya mbele ya basi letu huku nafungua macho naliona daraja likiwa mbele yetu na dereva akijitahidi kulenga kuvuka huku gari ikiwa ishapoteza mwelekeo kwa kasi aliyokuwa nayo kufidia muda wa masaa 3 aliyoyapoteza wakati tukiziba rejeta.
Gari iliyumba kwa kishindo na kasi kubwa ilivuka daraja na kupamia vizingiti vya barabara ambavyo huonyesha uelekeo wa daraja (hujengwa kama vinguzo vidogo viingi kabla ya daraja au kona kali vikiwa vimepakwa rangi nyeupe) na kuvibomoa kama vinne kabla ya kuyumba kwa kasi kubwa huku mayoe na kelele za vilio kwa akina mama na watoto vikifunika masikio yetu katika gari, waliomtaja Muumba wao kwa majina tofauti, Yesu na Mtume Muhhamad bila kumsahau mama walilia sana.


MUUJIZA AMBAO SIKUWAHI KUUONA
Haya yote yanatokea ni ndani ya kama sekunde 55 tu huku sasa tukiliona gari likielekea kuangukia mkono wa kushoto na katika kile ambacho mimi na abiria mwingine yeyote aliyeona hatakuwa na la kukwambia zaidi ya kusema ”MUNGU HANA MFANO WAKE”, Muda huu sasa gari inaanguka mkono wa kushoto na mie natazama paale ndo tunakwenda kulala sasa hatujui hii nguvu na huo msukumo uliotoka wapi baada ya gari kuwa kama imezuiwa na kitu na kisha kurudi mkono wa kulia wima na kusimama.
Kila mmoja anashuka katika gari na kumpongeza dereva huku wengine wakikimbilia katika vivuli vya miti wakitafakari. Dereva yeye akisogea kando kabisa ya barabara na kuoekana mwenye msongo mkubwa wa Mawazo. Ndipo likapatikana wazo kwamba walau watu wachache wenye hekima wamtulize kimawazo maana kwa msongo uliomkabili ghafla hakawii kuiangusha gari sasa rasmi.
DEREVA AFUNGUKA RASMI
Katika mazungumzo na dereva inabainika kuwa kumbe ni siku mbili zilizopita aligonga ngómbe kumi wa mmoja wa wafugaji wa kisukuma na katika hali ya kawaida hawakuafikiana vema juu ya fidia na ndipo yule mzee akawaambia sawa ”NENDENI ILA TUTAONA”
.
Hakuna mwenye hakika kama tukio hili linahusiana na kauili ya yule mzee ama la, ikabidi apigiwe simu na ndipo akaamua kuja katika eneo la tukio.
MZEE NAE ANENA
Kiumri haonekani kuwa mzee sana licha ya kuwa wao walikuwa wanamwita babu, ila wajihi wake unaonekana kuwa mtu asiye na chembe ya huruma katika nafsi yake kwa sie wenye karama za kusoma wajihi na tanbihi ya mtu.
Anafika na kauli yake ya kwanza inakuwa ”SI NILIWAAMBIA”, haongei maneno mengi anabembelezwa na jopo la abiria na anakubali kuruhusu gari iondoke kwa kulipwa ngómbe wake kidogo kidogo na anatoa shilingi 1500 na kumpa dereva (za nini hizi Mungu wangu)
Ajali yapishiliwa mbali na uwezo wa Allah
Haya ndio yaliyojiri katika tukio hili ambalo kama si kugharimu maisha yetu na abiria wenzangu lingetauacha katika vilema ama mejeraha makubwa sana. Gari ilikuwa kasi na tulivyonusurika ni kwa Uwezo na miujiza ya Allah.”
Tumshukuru Mungu kwa yote.
Yahya M

No comments:

Post a Comment