AZAM YASUFUKUZIA USUKANI WA LIGI
Michuano
ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea
kesho (Oktoba 24 mwaka huu) kwa mechi nne za raundi ya tisa huku Azam
ikiusaka usukani wa ligi hiyo ikiwa mwenyeji wa Ruvu Shooting.
Mechi
hiyo namba 60 ambayo kama Azam itashinda itafikisha pointi 20, hivyo
kuwa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom itachezwa Uwanja wa Chamazi, Dar
es Salaam. Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 3,000 kwa sh. 10,000.
Yanga
itawakaribisha Polisi Morogoro ambao ndiyo wa mwisho kwenye msimamo wa
Ligi Kuu ya Vodacom hivi sasa katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000
na sh. 20,000.
Alex
Mahagi kutoka Mwanza ndiye atakayepuliza filimbi kwenye mechi hiyo
namba 62. Waamuzi wasaidizi ni Frank Komba na Michael Mkongwa, wote
kutoka Iringa wakati mwamuzi msaidizi ni Oden Mbaga anayetambuliwa na
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wa Dar es Salaam.
Uwanja
wa Mkwakwani jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya African
Lyon ya Dar es Salaam ambao ni wageni wa Coastal Union inayonolewa na
Hemed Moroco. Nayo Mtibwa Sugar itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja
wa Manungu ulioko kwenye mashamba ya miwa Turiani mkoani Morogoro.
MTIBWA SUGAR, JKT RUVU SASA KUCHEZA NOV 7
Mechi
namba 79 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Mtibwa Sugar na JKT Ruvu
iliyopangwa kuchezwa Novemba 3 mwaka huu Uwanja wa Manungu mkoani
Morogoro, sasa itafanyika Novemba 7 mwaka huu.
Mabadiliko
hayo yamefanyika kwa vile Novemba 4 mwaka huu, Mtibwa Sugar itacheza
mechi namba 30 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.
Mechi hiyo awali ilikuwa ichezwe Oktoba 3 mwaka huu lakini ikabadilishwa
ili kutoa fursa kwa mechi za Super Week zilizooneshwa moja kwa moja na
kituo cha televisheni cha Super Sport cha Afrika Kusini.
VITAMBULISHO FAINALI ZA AFCON 2013 MWISHO NOV 7
Waandishi
wa Habari wanaotaka kuripoti fainali za mataifa ya Afrika (AFCON)
zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini wanatakiwa kutuma maombi ya
kupatiwa vitambulisho (Accreditation) kabla ya Novemba 7 mwaka huu.
Maombi
hayo yatumwe Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kupitia CAF
Medial Channel inayopatikana katika mtandao wa Shirikisho hilo wa www.cafonline.com
FDL KUANZA KUTIMUA VUMBI OKT 24
Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaanza kutimua vumbi kesho (Oktoba 24 mwaka huu) kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Kundi
A kutakuwa na mechi tatu ambapo Burkina Faso itacheza na Mbeya City
kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati JKT Mlale itakuwa
mwenyeji wa Small Kids kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea.
Nayo
Kurugenzi itaumana na Majimaji katika Uwanja wa Wambi ulioko Mufindi
mkoani Iringa. Kundi hilo litamaliza raundi ya kwanza keshokutwa (Oktoba
25 mwaka huu) kwa mchezo kati ya Mkamba Rangers na Polisi Iringa
utakaofanyika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Mechi
za kundi B kwa kesho ni Ndanda dhidi ya Transit Camp katika Uwanja wa
Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Villa Squad itakipiga na Moro United
kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi. Oktoba 25 mwaka huu ni Green
Warriors v Tessema (Mabatini, Mlandizi) na Polisi Dar v Ashanti United
(Uwanja wa Chamazi).
Kundi
C kesho (Oktoba 24 mwaka huu) ni Kanembwa FC v Polisi Dodoma (Uwanja wa
Lake Tanganyika, Kigoma), Mwadui v Morani (Kambarage, Shinyanga), Pamba
vs Polisi Mara (Kirumba, Mwanza) na Rhino Rangers vs Polisi Tabora (Ali
Hassan Mwinyi, Tabora).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment