Vurugu hizo ziliibuka Oktoba 17 mwaka huu baada ya kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMUIKI) Sheikh Farid Ahmed Hadi kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Oktoba 16, mwaka huu.
Kijana Salum Bakari Muya anayedaiwa kuteswa na Polisi |
Amesema kabla ya kukutwa na tukio hilo alikuwa amekaa na wenzake wakiwa wanasubiri tenda ya mizigo ya kusafirisha kwa kutumia magari ya punda.
“Nilikuwa nabangaya – yaani kubangaiza –wakatokea polisi sita, walipofika nilipokaa wakanifunua kofia na kunikata kipande cha ngozi na nywele kichwani kwa kisu,” alisema Salum.
Kipande cha sehemu aliyokatwa kijana huyo kwa kisu kabla ya kunyolewa |
Bw Salum amedai kuwa baada ya kupata matibabu katika kituo hicho cha JKU iliamriwa kwamba apelekwe Hospitali Kuu ya Mnazimoja kwa vile alikuwa anavuja damu nyingi.
Hata hivyo alisema alishangaa kabla ya kufika Mnazimoja polisi hao waliamua kumtekeleza katika eneo la kwa Abbas Hussein, lililopo kilometa chache kutoka walipomtoa hospitali ya JKU.
“Hawakunifikisha Manazimoja, wakaniacha na kuondoka huku wakisema ubaya ubaya mtakoma waambie na wenzio,” alisimulia Salum akiwa na bandeji aliyofungwa wakati anapata huduma ya kwanza.
Alisema baada ya kutelekezwa na polisi aliamua kwenda Welesi huko Kikwajini kwa lengo la kuzungumza na waandishi wa habari juu ya mkasa uliompata.
Baada ya kusimulia mkasa huo, Salum ambaye alifuatana na kaka zake walioomba wasiandikwe majina baadae alipelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi.
Alipoulizwa juu ya tukio hilo, Kamishana wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema bado hajapewa taarifa na kwamba iwapo mwathirika atalalamika kituoni polisi watachukua hatua ya kucunguza.
“Tumezoea kulalamikiwa, kama mtu amefanyiwa ukatili kwanini asiripoti kituo cha polisi, hapo ujue kuna jambo anaficha,” alisema Kamishna Mussa.
Lakini baada ya kuelezwa na mwamdishi wa habari hizi kwamba kijana huyo amepelekwa hospitali na kaka zake, Mussa alisema aliahidi kufuatilia tukio hilo.
Kitendo cha Salum kufanyiwa ukatili na watu wanaodaiwa kuwa polisi kimetanguliwa na matukio ya vijana wenguine wawili kuuawa wakati wa utekelezaji wa zoezi la msako huo mjini Zanzibar mwezi Oktoba mwaka huu.
Imedaiwa kuwa Hamad Ali Kaimu aliuawa Ijumaa iliyopitama wakati akiwa mikononi mwa polisi katika eneo la Magomeni na Salum Hassan Mahanju alikufa baada ya kupigwa risasi katika maeneo ya Amani Fresh na watu waliotajwa kuwa maofisa ulinzi na usalama.
Mbali na vijana hao, askari mmoja Koplo Said Abdulrahman aliuawa na watu wasiojulikana huko Bububu baada ya tukio la kutoweka Sheikh Farid.
Tokea kuanza kwa vurugu visiwani Zanzibar jumla ya watu watatu wamefariki ikiwa mmoja ameuwa na watu wenye hasira huku jeshi la polisi likidaiwa kuwaua vijana wawili
No comments:
Post a Comment