BAADA YA UTEUZI WA WAKUU WA WILAYA UTEUZI wa wakuu wa wilaya uliotangazwa juzi umezua mjadala baada ya watu wa kada tofauti wakiwemo wasomi, wanasiasa, wanaharakati na wananchi wa kawaida, huku wengine wakidai kwamba ni sehemu ya kulipana fadhili pia mpango maalum wa CCM kupanga safu yake katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Habari kutoka ndani ya CCM zinadai kuwa baadhi ya makada wanautizama uteuzi huo kama moja ya hatua za kuumiza kambi mojawapo ndani ya chama hicho, wakati kikielekea katika uchaguzi wake wa ndani ambao mchakato wake tayari umeanza. Hata hivyo, wakati wadau hao wakikosoa uteuzi huo, CCM kwa upande wake kimepuuza madai hayo na kuwataka wanaodhani kuna tatizo la kikatiba, kupeleka hoja zao kwenye Tume ya Kukusanya maoni ya Katiba Mpya, ili yafanyiwe kazi. Katika uteuzi huo, ambao Rais alifanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya zote nchini, wamo waandishi wa habari, wabunge wa viti maalumu na baadhi ya makada wa CCM walioangushwa kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi na wengine walioshindwa na wapinzani. Wabunge hao wa zamani ni Ponsiano Nyami, Suleiman Kumchaya, Dk Charles Mlingwa, Manju Msambya, Omar Kwaangw’, Venance Mwamoto, Benson Mpesya, Daudi Felix Ntibenda, Ramadhani Maneno, Gulamhusein Kifu na Esterina Kilasi. Habari kutoka ofisi ndogo ya CCM Lumumba na zile za makao makuu ya Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) jijini Dar es Salaam zinasema baadhi ya makada walipigwa na butwaa baada ya majina yao kutokuonekana katika orodha hiyo kwani walikuwa na matumaini makubwa. “Huwezi kuamini hapa kwetu leo wengine wanachekelea na wengine wamenuna…..kisa eti ni U-DC, kuna makundi yameumizwa, kwanza watu wao wameambulia patupu, lakini hata wengine waliokuwamo kwenye timu ya zamani wametoswa,”alisema mmoja wa makada wa chama hicho aliyepo CCM Lumumba. Habari kutoka Dodoma ambako pia kuna vikao vya Sekretarieti ya CCM zilidai kuwa baadhi ya makada wameanza kuhofia nafasi zao katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho baada ya wale waliokuwa wakidhaniwa kuwa watawatetea kuachwa katika uteuzi huo. Katiba ya CCM inawatambua wakuu wa wilaya kuwa wajumbe wa Kamati za Siasa za Wilaya, wakati wakuu wa mikoa ni wajumbe wa kamati za siasa za ngazi hizo. Kwa kuwa wajumbe hao ni wateule wa Rais hutizamwa ndani ya chama hicho kama watu muhimu ambao hulinda maslahi ya mamlaka zilizowateua, hivyo misimamo yao katika vikao hivyo huwa na nguvu kubwa ya ushawishi wa kimaamuzi. “Sasa wewe unadhani kwamba ukiwa unagombea uongozi wowote, halafu ukaona DC au Mkuu wa Mkoa anakupinga, ujue huo ndio msimamo wa Bwana mkubwa (Mwenyekiti wa Taifa ambaye pia ni Rais), kwa hiyo kama ulikuwa na mtu wako akatoswa ujue ndio hivyo mambo huenda yasiwe mazuri,”alisema kada mwingine aliyezungumza na gazeti hili makao makuu ya CCM mjini Dodoma jana. Vyama vya siasa Kwa upande wake vyama vya Chadema, NCCR – Mageuzi na CUF vilisema kwa nyakati tofauti kuwa havioni umuhimu wa kuwapo kwa wakuu wa wilaya na kwamba nafasi hizo ni kwa ajili ya kutoa ulaji kwa wanasiasa walioshindwa ndani ya CCM. Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kwa wale wasioridhishwa na uwapo wa wakuu wa wilaya wafikishe hoja zao kwenye Tume ya Marekebisho ya Katiba ili maoni yao yafanyiwe kazi. Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema kundi hilo la wateule wa Rais ni mzigo kwa nchi kwa sababu hawana kazi ya kufanya zaidi ya kuwajibika kisiasa. “Tunahitaji nini kutoka kwa Mkuu wa Wilaya, katika kila wilaya kuna madiwani wanaouchaguliwa na wananchi, wabunge na Meya ama mwenyekiti wa Halmashauri husika, kweli tunahitaji DC hapo?” alihoji. Aliongeza, “Pia kuna wakurugenzi wanaofanya kazi kwa niaba ya Serikali pamoja na watendaji wengine sasa hawa wakuu wa wilaya kazi zao zipi.” Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo alisema , “Chadema hatuwezi kupongeza uteuzi huo kwani hatutambui uwepo wao.”Mnyika alisema kimsingi, kundi hilo la wateule wa Rais halina kazi ya kufanya zaidi ya ile ya ujumbe katika Kamati za Siasa za Wilaya za CCM. Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Sam Ruhuza alisema Watanzania wanatakiwa kufuta vyeo vya Mkuu wa Wilaya katika Katiba Mpya ambayo mchakato wa kuiandaa umeshaanza. Alisema wateule hao mpaka sasa hawajulikani kazi wanayoifanya ni ipi kwa kuwa kila wilaya kuna mbunge, wenyeviti wa wilaya, meya wa manispaa, wakurugenzi na watendaji wengine ambao nao wakati mwingine utendaji wao umekuwa ukiibua migogoro. Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema chama chao hakioni umuhimu wa wakuu wa wilaya na kwamba hawana msaada wowote kwa wananchi bali wanalinda maslahi ya chama. "Wakuu wa wilaya ni makada tu wa chama hivyo ni muhimu wachaguliwe na si kuteuliwa tu na Rais kwa kuwa wanajipa mamlaka makubwa,"alisema Mtatiro. Alisema nchi haihitaji makada wa CCM ambao wameshindwa kwenye ubunge na kushindwa kazi maeneo mengine wawekwe kwenye nafasi muhimu kama hizo. "Wanakwenda kulinda maslahi ya CCM na si kuwasaidia wananchi. Ni bora hizi nafasi zifutwe au ziwekewe utaratibu wa kupatikana,"alisema Mtatiro. Wasomi na wanaharakati Mwanaharakati kutoka kituo cha Sheria na Haki za binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema wakuu wa wilaya na mikoa hawana tija yoyote na kwamba kazi wanazozifanya zinaweza kufanywa na wakurugenzi wa wilaya. Alisema uwepo wa wateule hao ni mwendelezo wa fikra za utawala wa kikoloni kwa kuwa wahusika hawawajibiki kwa wananchi bali kwa Rais aliyewateua. Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema uteuzi huo wa wakuu wa wilaya ni maandalizi ya CCM kukabiliana na Uchaguzi Mkuu wa 2015. Alisema kitendo cha kuteuliwa kwa wagombea wanne walioshindwa kwenye uchaguzi wa ubunge katika Uchaguzi Mkuu kupitia CCM kuwa wakuu wa wilaya ndio inalithibitisha hilo. “Mkoa wa Kigoma umetoa ma-DC ambao wameshindwa katika uchaguzi hii ni ishara kuwa CCM inajipanga kukusanya fedha kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015” alisema Kafulila. Walioteuliwa kushika nafasi hiyo ambao kwa kipindi tofauti walikuwa wabunge wa Jimbo la Kigoma Kusini ni Kifu Gullamhussein na Manju Msambya. Kafulila alisema kuwa Katiba Mpya itafuta kila kitu na hakutakuwa tena na Mkuu wa Wilaya ifikapo 2015. “Wakuu wa Wilaya kazi yao ni kupokea Mwenge wa Uhuru tu ambao hauna faida kwa Watanzania” alisema Kafulila. Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema uteuzi huo umelenga kuiimarisha CCM kutokana na vijana kupewa nafasi zaidi. Alisema hizo ni dalili kwamba CCM wameona nguvu ya upinzani na sasa wameanza kujiimarisha kwa kuwatumia vijana na wakuu hao wa wilaya. “Wamehofia kuwa wanaweza kwenda Chadema ndio maana wameamua kuwapa nafasi vijana, hiyo ni changamoto ambayo wameifanyia kazi” alisema Dk Bana. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema anachoona ukuu wa wilaya ni maalum kwa makada wa CCM waliokosa mahala pengine pa kwenda ni mwendelezo wa ufisadi. Akitolea mfano wa makada wawili wa CCM (majina tunayo) ambao sasa ni wakuu wa wilaya, Lissu alisema mmoja kati yao amepewa cheo hicho baada ya chama hicho tawala kumchakachua wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010. "Baada ya uchakachuaji huo … alijiuzulu. Uteuzi wa jana wa kada huyo ni ushahidi tosha kwamba U –DC aliopewa ni rushwa ya wazi wazi." Kwa upande wa Wakili Majura Magafu alisema anatarajia kuona wakuu wa wilaya hao wapya walioteuliwa hususani waandishi wa habari na wakili, wanatimiza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa haki na udilifu. “Mchakato huu wa uteuzi wa wakuu wa wilaya ulifanywa kwa umakini na Rais Kikwete, walioteuliwa wasichekelee bali wawajibike kwa wananchi ,hatutarajii kuwa wataondolewa kwa kashfa kama walioondolewa,” alisema Magafu. Aliwasisitiza kutimiza wajibu wao, akiwataka wasiwe wabinafsi wafanye kazi kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla ili wasije kumdhalilisha Rais na wale waliomshauri kufanya uteuzi huo. Wakili Patrick Ngayomela aliupongeza uteuzi huo na kuwataka wakuu hao wa wilaya walioteuliwa kukabiliana na changamoto nyingi zinazoikabili Serikali kwa sasa, akiwataka wawe mstari wa mbele kupambana na rushwa na ufisadi. Ngayomela alisema ili taifa liwe na maendeleo ni lazima watendaji wafanye kazi kwa ufanisi, uadilifu na wapambane na vitendo vyote vinavyoashiria kuwepo kwa matukio ya ufisadi na rushwa. Pia aliwataka waihamasishe jamii kutambua haki zao na kupambana na vitendo hivyo vinavyorudisha nyuma uchumi na maendeleo ya taifa. Tarime wamkataa DC Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Tarime limemkataa mkuu wa wilaya hiyo, John Henjewele kwa madai kuwa ameshindwa kusimamia masuala ya ulinzi na usalama hasa mauaji Mgodi wa Nyamongo. Msimamo huo umetolewa na madiwani wote 49 bila kujali itikadi za vyama vyao, hivyo kusababisha kushindwa kufanyika kwa kikao cha baraza lao, kilichokuwa mahususi kwa ajili ya kujadili taarifa CAG. Waligoma kufanya kikao hicho wakitaka awepo kwanza Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa ili waweze kumkabidhi mkuu huyo wa wilaya kwa maelezo kwamba hawamhitaji wilayani hapo . Pia walisisitiza kuwa kama hatatolewa, hawatakuwa tayari kufanya vikao vyovyote ama kupokea maagizo ya Serikali kupitia kwake kwa kuwa hawamtaki na anatakiwa kutafutiwa sehemu nyingine za kufanya kazi. Kauli za madiwani Mwenyekiti wa Kambi ya upinzani, Ndesi Charles Mbusiro ambaye ni diwani wa kata ya Turwa (Chadema), alisema azimio hilo ni la madiwani wote. “Ndani ya chama chake kama kada wamezungumza wameshindwa kuelewana ina maana hata vyombo vya usalama havimwambii Rais ukweli sasa wameleta kwenye baraza ambako ni wawakilishi wa watu tumekubaliana aondoke na hakuna mjadala na mkuu wa mkoa amearifiwa,”alisema. Anthony Manga kata Nyamaraga, (CCM) alisema ndani ya chama wamekwishamwita na kumweleza udhaifu wake, lakini ameshindwa kubadilika hasa masuala ya ulinzi na usalama, kuweka vizuizi ambavyo vinawanyanyasa wananchi kwa kuongeza rushwa . Miongoni mwa wakuu wa wilaya wapya yumo wakili wa zamani wa NSSF, Crispin Meela ambaye alisema ameupokea uteuzi huo kwa furaha, lakini anatambua changamoto zinazoikabili Serikali hususani za ubadhilifu wa fedha, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.“Kama mwanasheria katika nafasi hii nataka kuangalia na kujifunza sheria za tawala za mikoa na Serikali za mitaa zilizopo kama zinakidhi mahitaji kwa wakati uliopo kwa sababu zinamapungufu katika dhana ya mgawanyo wa kazi,”alisema Meela. Kwa hisani ya gazeti la Mwananchi |
FLASH
Friday, May 11, 2012
MAONI YA WANA ZUONI NA WADAU WA SIASA MARA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment