FLASH

Thursday, July 19, 2012

POSHO ZA WABUNGE ZA SIKU MOJA KUSAIDIA WAATHIRIKA WA AJALI YA MELI ZANZIBAR.
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania wamekubaliana kukusanya posho zao zote za siku moja na kutoa kama rambirambi kufuatia ajali ya meli ya Skagit iliyotokea Zanzibar tar 18/07/2012 katika kisiwa cha Chumbe

Spika wa bunge Bi Anne Semamba Makinda amesema bungeni mjini Dodoma leo asubuhi wakati akiahirisha bunge kufuatia ajali hiyo na kwamba bunge limeahirishwa mapema asubuhi kutokana na makubaliano yaliyofikiwa na kamati ya uongozi

Kabla Spika hajaahirisha bunge, waziri wan chi ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu na bunge Bw William Lukuvi alitoa taarifa ya serikali kuhusu majonzi na masikitiko kufuatia ajali hiyo
Meli ya Skagit ikiwa chini- juu
Amesema meli hiyo ilikuwa na abiria 290 wakiwemo watu wazima 250 na watoto 31
Bw Lukuvi amesema kuwa hadi kufikia leo asubuhi watu waliokuwa wameokolewa wakiwa hai walikuwa 146, maiti 31 na kwamba maiti hao wote wametambuliwa na ndugu zao

Aidha amesema ndani ya meli hiyo walikuwemo watalii 16 ambapo 14 kati yao wameokolewa wakiwa hai, mmoja amefariki na mwingine hajulikani aliko

Lukuvi amesema idadi ya wanaoendelea kutafutwa ni 113 na kwamba jana shughuli za uokoaji zilisimama kutokana na machafuko ya hali ya hewa na shughuli hizo zimeendelea leo
Waokozi wakiendelea na jitihada za kuwatafuta manusura na maiti pia
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilisitisha shughuli zake wakati siku hiyo ya julai 19 jioni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alitarajiwa kufanya majumuisho ya bajeti yake.

Aidha serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia leo Julai 19 hadi Julai 21

Akitangaza maombolezo hayo rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein ,amesema bendera zote zitapepea nusu mlingoti ikiwa ni pamoja na na kusitisha shughuli na sherehe zote za burudani kwa muda wa siku tatu za maombolezo.

Katika taarifa yake aliyoitoa Ikulu usiku wa kuamkia Julai 19, Rais Dk Shein amewahakikishia wananchi na hasa waliopoteza jamaa zao kuwa Serikali itabeba gharama zote za mazishi na pia kugharamia huduma za matibabu kwa majeruhi.
Baadhi ya maiti ambao tayari wamepatikana
Mbali ya taarifa hiyo, Rais Dk Shein aliungana na wananchi, viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, Viongozi wa dini katika kutambua maiti zilizofikishwa katika eneo maalum la viwanja vya Maisara Suleiman.

Baadhi ya Wabunge wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Mkuu wa Jeshi la Polisi wamewatembelea majeruhi katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na eneo la viwanja vya Maisara ambapo maiti hufikishwa kwa ajili ya utambuzi.

Mbali ya Bunge, pia Baraza la Wawakilishi Zanzibar lilisitisha kwa muda shughuli zake ili kutoa nafasi kwa Wawakilishi hao wa wananchi kushiriki katika shughuli za uokozi ambapo wengi walifika bandarini kusaidia kazi mbalimbali ikiwemo kuwafariji waliopoteza ndugu zao.
Wananchi pamoja na askari wa JKT wakiwa katika viwanja vya Maisara
Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 saa 7:50 mchana ikitokea Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikiwa imebeba abiria 250 watu wazima, watoto 31 na mabaharia 6.
Wakati huo huo Rais Jakaya Kikwete amemtumia salaam za Rambirambi rais wa Zanzibar Dr Ally Mohamed Shein akimpa pole kutokana na ajali hiyo ya pili mfululizo tangu aliposhika hatamu ya kuwa rais wa Zanzibar
 
Rais Kikwete katika taarifa yake amemwomba rais wa Zanzibar afikishe salaam za pole kwa wafiwa na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi ili wapone haraka na waendelee na shughuli za maendeleo

Rais Kikwete pia amepongeza hatua zilizochukuliwa na serikali ya Zanzibar katika  kutangazwa kwa taarifa za ajali hiyo pamoja na maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama na wafanyakazi wa meli kwa juhudi za uokoaji walizozifanya.

MTAZAMO;
Nami napenda kutumia fursa hii kutoa pole kwa Watanzania wote na hata mataifa ambayo ndugu zao walikuwemo kwenye meli hiyo kama watalii lakini pia nawasihi wataalam wa mamlaka ya Hali ya hewa nchini TMA kuwa makini zaidi na kutoa taarifa kwa wakati kuhusu hali ya hewa ili kuepuka ajali kama hiyo inayodaiwa kusababishwa na hali mbaya ya hewa

Aidha inadaiwa kuwa  TMA walitoa tahadhari sasa narudi kwa ndugu zetu wa mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu na majini SUMATRA kuwajibika kikamilifu na kuzuia vyombo visisafiri pale wanapokuwa na taarifa za tahadhari ya hali mbaya ya hewa kutoka TMA

Lakini pia setikali nayo iwe makini katika manunuzi ya vyombo hivi kwani inasemekana pia meli hiyo nayo haikuwa katika uimara/ubora wa kutosha kwa maana ilikuwa chakavu sijui niite mbovu, yote ni sawa tu

MUNGU  IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRICA

No comments:

Post a Comment